Skip Global Navigation to Main Content
Skip Breadcrumb Navigation
Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari

Watu wa Marekani wasaidia Miradi ya Kitanzania ya Maendeleo ya Jamii

Januari 16, 2013
Watu wa Marekani wasaidia Miradi ya Kitanzania ya Maendeleo ya Jamii (Picha: Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam)

Watu wa Marekani wasaidia Miradi ya Kitanzania ya Maendeleo ya Jamii.

Hapo tarehe 16 Januari, 2013 Balozi wa Marekani nchini Tanzania Alfonso E. Lenhardt alikabidhi ruzuku kwa mashirika 11 yanayolenga kuboresha maisha ya Watanzania na wakimbizi waishio nchini Tanzania. Jumla ya Dola za Kimarekani 97,635 (sawa na Shilingi za Kitanzania milioni 151) zimetolewa kama ruzuku kusaidia sekta za elimu, maendeleo ya kiuchumi, maji, nishati ya umeme wa jua na wakimbizi. Ruzuku hizi zinatolewa kama sehemu ya utekelezaji wa azma ya Marekani kushirikiana na Watanzania wanaoongoza jitihada za kuziletea jamii zao maendeleo kwa kutumia uongozi, mawazo na vipawa vyao wenyewe.

Mwaka huu Programu ya kusaidia vikundi na mashirika ya kijamii (Community Grants Program) imetoa ruzuku tano kutoka katika Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kujitegemea ya Jamii (Ambassador's Special Self-Help Fund), ruzuku moja kutoka Mfuko wa Julia Taft (kwa ajili ya kusaidia wakimbizi) na ruzuku tano kutoka katika Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI (Ambassador's Fund for HIV/AIDS Relief). Programu ya kusaidia vikundi na mashirika ya kijamiii inafadhiliwa na watu wa Marekani kwa kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa lengo la kutoa misaada midogo ya moja kwa moja kwa miradi ya kijamii inayolenga kuboresha maisha ya jamii husika.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeanzisha mifuko miwili ya utoaji wa ruzuku inayotoa ruzuku kila mwaka hapa Tanzania. Mifuko hiyo ni Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kujitegemea ya Jamii na Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI. Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kujitegemea husaidia miradi inayonufaisha jamii katika maeneo ya vijijini na mijini na Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI husaidia jamii ambazo zimeathiriwa zaidi au zilizo katika hatari zaidi ya kuathiriwa na janga hili. Mojawapo kati ya ruzuku zilizotolewa leo imefadhiliwa na mfuko wa Julia Taft wenye lengo la kusaidia wakimbizi, watu waliokimbia makazi yao na watu wasio na nchi (stateless persons).

Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kujitegemea ya Jamii ulianzishwa wakati wa muhula wa kwanza kwa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere. Kwa miaka 47 sasa mfuko huu umesaidia taasisi na vikundi vya kijamii kutoka kila mkoa wa Tanzania ili kuboresha Maisha ya Watanzania kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga shule, kuwezesha upatikanaji wa maji safi, matumizi ya nishati ya jua na uanzishaji wa miradi ya kuongeza kipato. Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI ulianzishwa miaka michache iliyopita na hadi sasa umetoa ruzuku kwa vikundi vya kijamii 49 nchini Tanzania. Mifuko hii inaendeleza utamaduni wa ushirikiano kati ya raia wa Marekani na Tanzania.

Katika hotuba yake, Balozi Lenhardt aliwapongeza wale wote waliopata ruzuku hizo na kusema kuwa "leo tunasherehekea uongozi na mawazo ya Watanzania ambao wanafanya jitihada kubwa na kujitoa kwa dhati kuendeleza miradi mbalimbali ya kijamii inayoboresha maisha ya Watanzania wenzao, hususan wale wanaohitaji msaada. Watu wa Marekani wamedhamiria kwa dhati kushirikiana na viongozi wa Kitanzania kama ninyi mliopo hapa asubuhi ya leo, kwa lengo la kusaidia jitihada na malengo yenu ya kupata ufumbuzi kwa Changamoto zinazoikabili Tanzania."

Ruzuku kutoka katika Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kujitegemea imetolewa kwa vikundi vitano. Taasisi iitwayo Indigenous Education Foundation of Tanzania imepata ruzuku kwa ajili ya kutekeleza programu ya ujasiriamali katika Shule ya Sekondari ta Okeeswa mkoani Arusha. Kikundi kiitwacho Tekla Kagera group kimepewa ruzuku kwa ajili ya kutoa elimu na kuwawezesha wanawake hususan, kwa kutoa mafunzo ya kompyuta na ushonaji kwa wasichana na wanawake wenye ulemavu mkoani Kagera.

Katika sekta ya elimu na maji, taasisi iitwayo Bright Light Organization ya mkoani Geita imepewa ruzuku kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha michezo kwa watoto wa shule ya awali na ujenzi wa mfumo wa uvunaji maji ya mvua shuleni hapo.

Katika eneo la maendeleo ya kiuchumi, taasisi iitwayo Continental Farmers Association ya mkoani Mara imepewa ruzuku kwa ajili ya kununua mashine mpya ya usagaji nafaka kwa lengo la kuboresha mradi wao wa usagishaji. Shule ya Msingi Utelewe ya huko Njombe imepewa ruzuku kwa ajili ya kuweka mfumo wa umeme utokanao na nishati ya jua katika shule yao.

Kupitia Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na UKIMWI, ruzuku inatolewa kwa miradi mitano ya kusaidia yatima na watoto waishio katika mazingira magumu pamoja na watu wanaoishi na VVU/UKIMWI.

Katika sekta ya elimu, ruzuku inatolewa kwa Shirika la Masista wa Theresia wa Mtoto wa Yesu ambalo litawasaidia watoto yatima na walio katika mazingira magumu wapatao 40 mkoani Kagera kwa kuwapatia vifaa vya shule. Aidha, ruzuku ya aina hiyo imetolewa kwa taasisi iitwayo Marilynn Orphans Projects Foundation, ambayo itajenga jiko na bwalo katika Shule ya Sekondari ta Mwaji kwa ajili ya watoto yatima mkoani Mbeya.

Katika sekta ya maji, Kanisa la Mennonite Tanzania huko Morogoro limepata ruzuku kwa aajili kuzisaidia kaya 260 zenye watoto yatima na watu wanaoishi na VVU/UKIMWI kutekeleza mradi wa kuchuja na kusafisha maji (water filtration) katika nyumba zao. Nayo Hospitali ya Mwambani iliyopo mkoani Mbeya imepata ruzuku kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu ili kuipatia hospitali hiyo maji.

Kikundi kiitwacho THYROID Group cha mkoani Morogoro kimepata ruzuku kwa ajili ya mradi wa wa kuweka mfumo wa nishati ya umeme wa jua katika kituo cha afya cha Kolelo.

Hali kadhalika, kwa kupitia mfuko maalumu wa kusaidia wakimbizi ujulikanao kama Julia Taft Fund for Refugees, ruzuku imetolewa kwa taasisi iitwayo Asylum Access kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi walio magerezani kupata huduma za kisheria. Mfuko wa Julia Taft Fund for Refugees unaendeshwa na Kitengo cha Idadi ya Watu, Wakimbizi na Uhamiaji cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ili kusaidia jamii za wakimbizi duniani kote. Mfuko wa Balozi wa Kusaidia Miradi ya Kujitegemea ya Jamii na Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na UKIMWI ni sehemu ya programu ya Balozi wa Marekani ya kutoa ruzuku kwa miradi mbalimbali ya kijamii. Kwa maelezo zaidi kuhusu programu hii kufahamu, tafadhali tembelea ukurasa wetu katika tovuti ya Ubalozi wa Marekani au wasiliana na Afisa wa Ubalozi Anayeshughulikia Ruzuku kwa anuani ya barua pepe selfhelpd@state.gov au kwa barua kupitia S.L.P 9123, Dar es Salaam.