VOANews.com

Sauti ya Amerika ▪ SwahiliPata habari za kuaminika

11 Januari 2009 

Leo VOA:

Habari katika Lugha 45
Hawa ni watangazaji wako ambao umekuwa ukiwasikia kwenye matangazo ya Sauti ya Amerika.

 

Mwamoyo Hamaza

Mwamoyo Hamza, Mkuu wa Idhaa

Mwamoyo Hamza ni mtangazaji wa siku nyingi katika Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika. Mzaliwa wa Tanga, Tanzania, Mwamoyo alisomea uandishi
habari katika Chuo Cha Uandishi wa Habari cha Dar es Salaam, Tanzania na kuanza kazi ya uandishi katika magazeti ya Daily/Sunday News. Baadaye alipata shahada za juu katika uandishi na mawasiliano katika chuo kikuu cha Howard mjini Washington D.C. Alijiunga na VOA mwaka 1994. Mbali na vipindi vya habari Mwamoyo pia anatayarisha makala za kila wiki za "Amerika Leo" na "Jamii na Maendeleo."


Abdushakur Aboud

Abdushakur Aboud
 

Abdushakur ni mtangazaji wa muda mrefu aliyejiunga na VOA 1992. Yeye ni mzaliwa wa Zanzibar lakini anatokea visiwani Comoro. Alihitimu uandishi wa habari katika chuo kikuu cha Dakar, Senegal, na kupata mafunzo ya utangazaji wa Televisheni huko Ujerumani na Japan. Alifanyakazi na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani, na baadae idhaa ya kiswahili na kingereza ya redio ya Uingereza BBC. Hivi sasa hutayarisha vipindi vya televisheni vya VOA pamoja na vipindi vya "Maswali na Majibu" na Muziki kutoka Afrika."


Ester Githui Ewart

Esther Githui Ewart

Esther Githui Ewart  ni mtangazaji katika idhaa ya Kiswahili  na televisheni ya Sauti ya Amerika . Ni mzaliwa wa Kenya ambaye alisomea uandishi habari katika chuo kikuu cha Nairobi. Kabla ya kujiunga na Chuo hicho alisomea shahada ya elimu katika chuo kikuu cha Kenyatta na kufundisha  kwa muda mfupi katika shule mbalimbali za sekondari nchini Kenya . Anafahamika vyema nchini humo ambapo kwa muda wa miaka minane aliandaa vipindi na kusoma taarifa za habari katika shirika la kitaifa la  televisheni na radio - K.B.C. Esther alijiunga na  Sauti ya Amerika  mwaka  2000. Mbali na kazi za kila siku za kuandaa ripoti na taarifa za habari, ni mhariri na mwandalizi wa kipindi kinachopendwa  sana “Jarida la Jumapili” ambapo huwaletea mahojiano ya kina  ya kijamii, kisiasa  kiuchumi na kitamaduni akiwaalika washiriki mbalimbali kutoka maeneo ya Afrika ya Mashariki; ya kati, Marekani na kwingineko . Amewahoji maafisa wakuu wa  serikali ya Marekani juu ya sera ya Marekani kwa Afrika mkiwemo  rais George W. Bush mwaka wa 2002 katika ikulu ya White House,  Rais mteule Barack Obama wa Marekani, mbunge Maxine Waters wa California miongoni mwa wengine. Kwa starehe zake  Esther anapenda kupumzika na  familia yake,  kusoma na kufuatilia matukio mbalimbali kupitia  vituo vya  televisheni.


  

Khajida Riyami

Khadija Riyami 

Khadija Riyami alijiunga na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika mwaka 1998. Kabla ya hapo alikuwa ni Mhariri wa Michezo katika magazeti ya Daily News/Sunday News nchini Tanzania.  Pia aliwahi kuwa mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani - Deutschewell na mwandishi wa kipindi cha michezo cha Fast Track katika Shirika la Utangazaji la Uingereza - BBC. Khadija hivi sasa ni Mhariri na pia anaandaa vipindi vya Dunia ya Wanawake na Matukio ya Afrika. alipata shahada ya uandishi kutoka Chuo cha waandishi wa habari nchini Tanzania na kupata mafunzo ya juu ya uandishi nchini Afrika Kusini, Ujerumani na Uingereza.


  
sunday

 

 

Sunday Shomari

Sunday Shomari ni mzaliwa wa Daressalaam Tanzania na alianza kazi ya utangazaji katika kituo cha radio one na ITV mjini Daresalaam akiwa anatangaza Muziki kwenye Televisheni hiyo na vipindi mbalimbali kwenye radio.Baadaye alifanya kozi ya utangazaji Marekani na kujiunga na chuo cha uandishi wa habari Tanzania na pia kuandika makala za burudani katika magazeti ya Nipashe na Alasiri na hivi sasa anaendelea na shahada ya mawasiliano katika chuo kikuu cha Maryland. Alijiunga na Sauti ya Amerika 2008 ambapo mbali na vipindi vya habari anaandaa kipindi cha Burudani kila Jumamosi.

 

 

 amon oscar

Amon Oscar

Amon Myimbili Oscar alijiunga na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika mwaka 2008 baada ya kuhitimu shahada ya juu ya mawasiliano katika chuo kikuu cha Northern Kentucky Marekani. Kabla ya hapo, alisoma katika chuo hicho hicho na kutunukiwa shahada ya uandishi habari mwaka 2006. Mwaka 1999 alipata stashahada ya uandishi habari kutoka St. Augustine University of Tanzania (SAUT), chuo cha uandishi wa habari kilichopo mkoani Mwanza nchini Tanzania. Alifanya kazi na Radio Tumaini mjini Dar es Salaam, na kupata uzoefu zaidi wa kazi ya uandishi kutoka makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York. Mbali na kazi yake  ya uandishi anapenda kusoma vitabu na kutembelea maeneo ya misitu, chemichemi za maji na bustani za maua..

  
timothy kaberiaTimothy Kaberia

Timothy Kaberia alijiunga na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika mwaka 2008. Mzaliwa wa Kenya, Kaberia alisomea siasa na lugha nchini ya Kenya na Marekani. Kabla ya kujiunga na Sauti ya Amerika, Kaberia alikuwa mratibu wa habari katika chuo kikuu cha American University, Washington, D.C. Alianza kazi ya utafiti na uandishi katika Tume ya Haki binadamu ya Kenya (KHRC) na baadaye akajiunga na kituo cha televisheni na redio cha Citizen mjini Nairobi kama ripota. Pia aliwahi kuwa mfasiri wa mashirika mbalimbali ikiwa ni pamoja ni kituo cha sheria na Amnesty International. Kaberia alipokea shahada ya BA (Honors) kutoka chuo kikuu cha Moi, Kenya. Alipokea mafunzo ya uandishi na mawasiliano nchini Burkina Faso na Marekani. Baadaye alipata shahada za juu katika uhusiano wa masuala ya kimataifa katika chuo kikuu cha American University mjini Washington, D.C.